Tuesday, 29 December 2015

Waliojenga vyanzo vya maji wapewa siku 21

Image result for Richard Kasesela
MKUU wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesera
MKUU wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesera ametoa siku 21 kwa watu wote waliojenga nyumba katika hifadhi au maeneo ya barabara na karibu na vyanzo vya maji, kubomoa kabla kazi hiyo haijafanywa na mamlaka zinazohusika. Kasesera alitoa agizo hilo Desemba 24 alipokuwa akijibu risala ya wananchi wa kijiji cha Igwachanja, nje kidogo ya Manispaa ya Iringa, walioomba wadau wawasaidie kujenga zahanati na kituo cha Polisi kijijini hapo.
Risala hiyo ilisomwa na Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Charles Matunduru wakati Mkuu wa Mkoa wa Iringa alipoweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda cha kutibu nguzo za umeme na bidhaa nyingine zitokanazo na miti, kinachojengwa na kampuni ya Agora Wood Products Ltd wilayani humo.
“Kwa kupitia hadhara hii, nawatangazia wote waliojenga nyumba katika maeneo yasiyoruhusiwa kisheria, iwe ndani ya barabara au katika maeneo mengine yasiyoruhusiwa; wale wanaolima au kufanya shughuli mbalimbali kama vile uchomaji wa tofali karibu na mito, natoa siku 21 wawe wameondoka,” alisema Kasesera.
Alisema baada ya siku hizo 21, serikali itatumia rasilimali zake kubomoa maeneo hayo na wanaohusika watapaswa kufidia gharama zake. “Kwa wale walioko karibu na mito, wajue sheria inataka wafanye shughuli zao mita 60 kutoka katika kingo za mito, kwa hiyo natoa mwito kwao waanze kuondoa vitu au mali zao zilizopo ndani ya mita hizo,” alisema.
Alisema serikali ya awamu ya tano, itasimamia utekelezaji wa sheria zote, ikiwemo sheria ya mazingira ili kuyalinda mazingira hayo kwa ajili ya vizazi vilivyopo na vijavyo.
“Ukiugua lazima sindano ichomwe panapohusika, iingie vizuri ili upone, ambianeni wote mliojenga barabarani, maeneo yasiyoruhusiwa au yenye matatizo kisheria, wachoma tofali, wakulima na wengineo, kwamba bomoeni au ondokeni kabla sindano haijawafikia,” alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Akijibu maombi ya wananchi wa kijiji hicho, Kasesera alivitaka vijiji kupunguza ombaomba kwa wawekezaji, akisema tabia hiyo wakati fulani inapunguza mahusiano na wawekezaji hao. “Tutumie nguvukazi tuliyonayo kujenga miradi ya maendeleo katika vijiji vyetu. Ujenzi wa zahanati na kituo cha Polisi unahitaji kwanza nguvu za wananchi wenyewe kabla wadau wetu wa maendeleo hawajaombwa kuchangia,” alisema.

No comments:

Post a Comment