Wednesday, 30 December 2015

Majaliwa ataka weledi Serikali za Mitaa



Image result for majaliwa




WATUMISHI wa Serikali za Mitaa wametakiwa kufanya kazi kwa kujituma wakizingatia maadili na taaluma zao badala ya kufanya kazi kwa woga na kwamba hakuna mtumishi yeyote atakayeadhibiwa akifanya kazi yake kwa weledi.
Ushauri huo ulitolewa jana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipozungumza na Wakurugenzi na Wakuu wa Idara kutoka halmashauri zote za mkoa Kigoma, wabunge na wakuu wa wilaya katika kikao cha maelekezo ya kazi akiwa katika ziara yake ya kwanza ya kiserikali tangu kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Waziri Mkuu.
Alisema kikubwa ambacho watumishi wa umma na serikali za mitaa wanapaswa kuzingatia ni utekelezaji kwa vitendo maagizo ya Rais Magufuli kwa kuzingatia maadili ya kazi, taaluma na uzalendo.
Ametaka watumishi kuzingatia mipango ya utendaji kazi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya wananchi iliyopo kwenye utekelezaji wa shughuli za halmashauri, mipango inayoambatana na bajeti zilizotengwa na halmashauri husika.
Pia amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri kuzingatia muda wa kuingia kazini kwa watumishi, muda wa kutoka na muda wanaoutumia wakiwa maeneo ya utekelezaji wa miradi na tija iliyoletwa kulingana na muda uliotumika.
“Mtumishi wa umma na serikali za mitaa hana sababu ya kufanya kazi kwa woga kama kweli anatimiza majukumu yake katika kuwatumikia Watanzania, lakini kama huendani na utendaji wenye uadilifu, unaozingatia taaluma na kujituma huyo hatutamwacha na ndiyo tunaotaka kuwaondoa katika utekelezaji wa majukumu yetu,” alisema.
Katika kuonesha kila mmoja anawajibika kwa mwingine, Majaliwa alisema Tamisemi ambayo ndiyo kiini cha utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya nchi, itaandaa vigezo na majukumu ya utekelezaji wa shughuli zao kwa Wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuondoa utendaji kazi wa mazoea.

No comments:

Post a Comment