Monday, 21 December 2015

CCM washinda ubunge Masasi, Ludewa wanukia

 Image result for abdulrahman kinana



CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeendelea kutamba katika chaguzi ndogo baada ya kushinda katika Jimbo la Masasi mkoani Mtwara huku ikiwa na kila dalili ya kutangazwa mshindi Ludewa mkoani Njombe.
Katika chaguzi saba zilizofanyika baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, CCM imezoa viti sita huku kimoja cha Kijitoupele mjini Unguja kikisubiri tarehe mpya ya uchaguzi.

CCM imeshinda katika majimbo ya Lushoto, Handeni Mjini, Lulindi, Ulanga Mashariki, Masasi na Ludewa ambayo ingawa matokeo rasmi yalikuwa hayajatangazwa wakati tukienda mitamboni, lakini CCM ilikuwa ikiongoza kata 20 na zilikuwa zimebaki kata sita.

CCM imepoteza tena Jimbo la Arusha Mjini. Mgombea ubunge Jimbo la Masasi kupitia CCM, Rashid Chuachua ameibuka kidedea kwa kupata ushindi katika uchaguzi huo mdogo juzi kwa kumshinda mpinzani wake wa karibu kutoka Chama cha Wananchi (CUF).

Uchaguzi huo mdogo wa ubunge ulifanyika kutokana na kushindwa kufanyika Oktoba 25 baada ya mgombea ubunge wa jimbo hilo wa chama cha NLD, Dk Emmanuel Makaidi kufariki dunia Oktoba 15, mwaka huu katika Hospitali ya Misheni ya Nyangao mkoani Lindi kutokana na tatizo la shinikizo la damu.
Akitangaza matokeo hayo usiku wa kuamkia jana, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Masasi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Masasi, Fortunatus Kagoro alisema wananchi 60,598 waliandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, huku Chuachua akipata kura 16,597 na mpinzani wake wa karibu kutoka CUF, Ismail Makombe (Kundambanda) akipata kura 14,069.

Wagombea wengine ni Mustapha Swalehe wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alipata kura 512, Dk Peter Mrope wa ACT- Wazalendo kura 347 huku mgombea wa NLD akiambulia kura 70 pekee.

Wakala wa CUF ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma alisema mgombea wao ameshindwa kwa kura na kwamba Tume ya Uchaguzi imetenda haki kwa kuendesha uchaguzi wa uwazi na ukweli kuanzia kwenye vituo vya upigaji kura hadi kwenye majumuisho ya matokeo.
Katika Jimbo la Ludewa, mgombea wa CCM, Deo Ngalawa amewaacha kwa mbali wagombea wengine katika matokeo ya kata 20 zilizokuwa matokeo yake yamepatikana.

No comments:

Post a Comment