IDADI ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaoomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Uspika na Unaibu Spika katika Bunge la 11 linalotarajiwa kuanza wiki ijayo, inazidi kuongezeka ambapo hadi sasa wamechukua fomu wanachama takribani 21.
Kati ya wanachama wapya waliochukua fomu jana ni pamoja na aliyekuwa Naibu Spika katika Bunge la 10 na Mbunge mteule wa Kongwa, Job Ndugai, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Tulia Arkson na aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi.
Kwa mujibu wa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayeshughulikia Oganaizesheni, Muhammed Seif Khatib, kwa siku ya jana pekee takribani wanachama 10 walichukua fomu za kuwania nafasi hiyo.
Juzi ambayo ilikuwa siku ya kwanza kwa mujibu wa ratiba ya chama hicho kwa wanachama wanaotaka kuomba kuteuliwa kuwania nafasi hizo, pia walijitokeza makada 10 waliochukua fomu akiwemo Spika mstaafu, Samuel Sitta.
Hata hivyo, jana pia ilikuwa ni siku ya mwisho ya kuchukua fomu hizo na kuzirejesha kwa wanachama wanaoomba kuteuliwa kuwania nafasi hiyo ambao si wabunge. Kwa wanachama ambao ni wabunge wateule, mwisho wa kuchukua na kurejesha fomu hizo ni keshokutwa.
Khatib aliwataja wanachama wengine waliochukua fomu hizo jana kuwa ni Mbunge mteule wa Chato, Dk Medard Kalemani, Diwani wa Goba jijini Dar es Salaam, Mwakalika Watson, Julius Pawatila, Agnes Makune na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdullah Ali Hassan Mwinyi.
Wengine ni aliyewahi kuwa Naibu Waziri, Ritha Mlaki na mhitimu wa chuo kikuu mwenye umri wa miaka 28, Veraikunda Urio. Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu hizo, Ndugai alisema ameamua kuwania nafasi hiyo kutokana na ukweli kuwa Bunge la 11 ni Bunge litakalokuwa na changamoto hivyo linahitaji Spika mwenye weledi, uvumilivu na uzoefu wa kutosha katika mambo ya kuongoza Bunge.
“Mimi nina uzoefu wa zaidi ya miaka 10 ninazifahamu vyema Kanuni za Bunge na matumizi yake, lakini pia nimeshiriki katika mabunge mbalimbali likiwemo Bunge la Jumuiya ya Madola. Ninachoweza kuahidi ni utumishi uliotukuka,” alisema Ndugai.
Kwa upande wake, Dk Masaburi alisema anaamini kati ya wanachama waliojitokeza kuwania nafasi hiyo, yeye ana sifa kuliko wote kutokana na ukweli kuwa pamoja na uzoefu alionao, pia ni msomi aliyebobea katika masuala mbalimbali ya uongozi na masuala ya ununuzi na uchumi.
“Mimi nina taaluma ya ufundi, usimamizi wa masuala ya usafiri, taaluma ya ununuzi na uhasibu ngazi ya cheti, nina utaalamu katika masuala ya mikataba ya ununuzi na lengo langu ni kuhakikisha bajeti inayopangwa na Serikali inaendana kwanza na mipango ya manunuzi kabla ya kupitishwa,” alisema Masaburi.
Alisema ana uzoefu mkubwa katika masuala ya uongozi kwani ameongoza Jiji kama Meya kwa takribani miaka 10, aliwahi kuwa Mbunge wa Afrika Mashariki na pia Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT).
Naye Mlaki alisema anatambua kuwa Bunge la 11 litakuwa na changamoto kutokana na kuwa na wabunge wengi wapya ambao ni zaidi ya 1/3 ya wabunge wote, hivyo Bunge hilo litahitaji Spika makini, asiye mwoga na mwenye kuzingatia haki.
“Nimechukua fursa hii kwa sababu nimekuwa mbunge kwa miaka 10, lakini pia nimewahi kuwa Waziri wa wizara mbalimbali. Nikiwa bungeni nimeshiriki kupitisha miswada mbalimbali ambayo baadaye huwa sheria, dhamira yangu ni kuhakikisha kuwa Bunge la 11 linaongeza umakini katika kupitisha miswada hii,” alisisitiza Mlaki.
Wanachama 10 waliojitokeza kuchukua fomu juzi pamoja na Sitta ni aliyekuwa Mbunge wa Karagwe, Gosbert Blandes na aliyekuwa mmoja wa wagombea takribani 42 waliojitokeza kuwania nafasi ya Urais ndani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Dk Kalokola Muzzamil.
Wengine walikuwa Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi; aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge Philip Marmo; Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, Mbunge wa zamani wa Afrika Mashariki, George Nangale, Simon Rubugu, Banda Sonoko na Leonce Mulenda.
No comments:
Post a Comment