Sunday, 22 November 2015
VITANDA 300 MUHIMBILI VYANUNULIWA KWA FEDHA ZA HAFLA
FEDHA za hafla ya wabunge ambazo Rais John Magufuli aliagiza zipelekwe katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, zimewezesha kununua vitanda 300 vya wagonjwa.
Shilingi milioni 251 zilikabidhiwa kwa Bohari ya Dawa (MSD) ambayo nayo haikutaka kuchelewa na ikanunua vitanda hivyo 300 ambavyo vilishushwa juzi katika hospitali hiyo.
Akizungumza kuhusu swala hilo Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Lauren Bwanakunu alikiri kuwa kweli vitanda hivyo vimenunuliwa na sehemu ya fedha kiasi cha Sh milioni 225 ambazo zilichangwa na wadau mbalimbali kwa ajili ya kugharamia hafla ya wabunge siku ya uzinduzi wa Bunge hilo juzi.
Bwanakunu alisema mbali na vitanda hivyo 300, pia wamenunua na kukabidhi hospitalini hapo magodoro 300, viti maalumu vya wagonjwa 30, vitanda vya kubeba wagonjwa 30 na mashuka 1,695.
“Ni kweli tumepeleka vitu hivyo Hospitali Taifa, tunakimbizana na mbio za Rais, sisi tulivyopokea tu fedha hatukutaka kuchelewa, tukanunua na kupeleka hospitalini mara moja, na ndio tutakavyokuwa tukifanya kazi kwa mchaka mchaka huo ili twende na kasi ya Rais,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema pia jana usiku walikuwa wanatarajia vifaa vya mashine ya MRI na CT-Scan kuwasili usiku jana kwa ndege ya Shirika ya KLM kutoka nchini Uholanzi na kuwa vingepelekwa moja kwa moja Muhimbili ambapo leo mafundi watavifunga.
Rais Magufuli juzi baada ya kulihutubia na kulizindua Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alihudhuria hafla fupi ya wabunge na kutoa agizo la fedha za shughuli kwa ajili ya uzinduzi wa bunge kupelekwa Muhimbili na kununulia vitanda vya wagonjwa baada ya kupokea taarifa kuwa wadau mbalimbali wamechanga kiasi cha Sh milioni 225.
“Nilipoambiwa kwamba zimechangwa Sh milioni 225 zimekusanywa kwa ajili ya sherehe, nikasema fedha hizo zipelekwe Muhimbili zikasaidie kununua vitanda… kwa kufanya hivi tutakuwa tumejinyima sisi wenyewe lakini tutakuwa tumewanufaisha wenzetu ambao wana matatizo makubwa yanayoweza kutatuliwa kwa fedha hizo,” alisema Dk Magufuli.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment