Wednesday, 11 November 2015

Ban Ki-moon asema magufuli ataleta maendeleo tanzania

 
Image result for ban ki moon
Ban Kimoon
 KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Kimoon ameeleza imani yake kwa Rais John Magufuli akisema chini ya uongozi wake, Serikali ya Tanzania itashughulika na juhudi za kuondoa umaskini, kuimarisha utawala na kupigania amani na utulivu katika Afrika Mashariki na nje ya ukanda.

Aidha, Mtendaji huyo wa Umoja wa Mataifa, amesema ana imani kuwa masuala ya uchaguzi yaliyobakia yatashughulikiwa kupitia taratibu za kisheria zilizopo kwa njia ya amani na uwazi.

“Napenda kukuhakishia kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kukuunga mkono pamoja na Serikali yako katika juhudi hizi,” alisema Ban kwenye barua yake ya pongezi aliyomtumia Dk Magufuli kutokana na kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Tano wa Tanzania mwishoni mwa mwezi uliopita.

Akizungumzia Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Ban alisema ni uthibitisho wa wazi na dhamira ya muda mrefu inayoonesha demokrasia, amani na utulivu wa Watanzania. “Nina imani kuwa masuala ya uchaguzi yaliyobakia yatashughulikiwa kupitia taratibu za kisheria zilizopo kwa njia ya amani na uwazi,” alisema Katibu Mkuu wa UN.

Ingawa hakutaja moja kwa moja masuala ya uchaguzi yaliyobakia, Mtendaji huyo wa UN alimaanisha uchaguzi wa Zanzibar ambao Tume ya Uchaguzi (ZEC) ilifuta matokeo yake baada ya kubaini kasoro kadhaa. Katibu Mkuu huyo wa UN ameipongeza Tanzania kwa kuwa mwenza imara na wa kutumainiwa wa Umoja wa Mataifa kwa miongo yote.

“Nathamini ushirikiano uliopo baina ya Umoja wa Mataifa na nchi yako na katika kuendeleza malengo ya UN, nakutakia mafanikio katika kutekeleza shughuli zako,” alisema. Kwa upande wake, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Kabwe Zitto, amepongeza hatua zilizoanza kuchukuliwa na Dk Magufuli tangu kuapishwa kwake hasa katika kusitisha safari za nje kwa viongozi serikalini.

“Tunapongeza hatua ambazo zimeanza kuchukuliwa na Rais mpya wa nchi yetu na hasa suala zima la kudhibiti safari za nje. Kwenye Bunge la 10 nilipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya PAC niliagiza ukaguzi kuhusu safari za nje na muda mwafaka utakapofika, tutatoa kwa umma taarifa hiyo ili wananchi wajue.”

Mtindo wa Magufuli unafaa. Watu wasimhukumu, lazima aoneshe yupo na huu ni uongozi wa Serikali nyingine…. Ameanza kwa kutembea kujua matatizo kabla ya kuunda Serikali,” alifafanua Zitto alipozungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Zitto alisema ziara hizo za Rais za kushitukiza pekee hazitatosha kutatua ubadhirifu na uvivu, bali lazima kuimarisha mifumo na kuhakikisha vitu vyote vinakaa kwa sheria na kanuni ili hata mtu mwingine akiingia madarakani aendeleze na kudhibiti.

Alisema wananchi wamekuwa wakiuliza taarifa hiyo ya safari za viongozi ni fedha kiasi gani zinatumiwa na Serikali na kama kuna uwezekano wa kuziokoa. Alisema ukaguzi uko tayari na watauweka wazi wananchi wajue ni gharama kiasi gani kwa wanasiasa na watendaji kwenda nje.

Kuhusu sakata la Zanzibar, Zitto alisema ACT-Wazalendo inamtaka Rais Magufuli kutoa kipaumbele katika suala hilo kwa kuwa jambo hilo ni nyeti pia kama mambo mengine ambayo ameanza kuyashughulikia.
Zitto aliwashukuru pia wananchi pamoja na uchanga wa chama, lakini kimekuwa chama cha tatu baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vinavyounda Umoja wa Katiba (Ukawa) katika kura za Urais.

“Hii yote ni heshima ambayo Watanzania wametupa na pia tunashukuru wana habari kwa kuuhabarisha umma nini ambacho tulikuwa tukifanya katika kipindi chote cha uchaguzi, tulimaliza na mgombea wetu wa urais alimkabidhi Rais Ilani yetu ya chama na hiyo ni ishara kwamba tumemtambua na tungependa aangalie yale ambayo tunayo ni yapi anaweza kufanya,” alisema Zitto.

Alimpongeza mgombea urais wa chama hicho, Anna Mghwira kwa kazi aliyoifanya kuzunguka nchi nzima kutafuta kura na kuwa mshindi wa tatu pamoja na wagombea wengine ambao walikuwa ni wanaume, jambo ambalo limemjengea heshima kubwa na kupandisha taswira ya chama mbele ya umma.

Aidha, alisema ACT-Wazalendo wamepata mbunge mmoja ambaye ni yeye kupitia Jimbo la Kigoma Mjini ambalo pia wamepata viti 12 vya udiwani kati ya 18 vilivyopo na kuahidi kutumia kiti hicho kupaza sauti ya chama ndani ya Bunge na kusimamia yale ambayo yalisimamiwa kwenye kampeni.

“Mtakumbuka chama chetu ndiyo chama pekee ambacho kiliweza kuzungumza sio tu ufisadi, lakini na majawabu yake, kwamba ni nini ambacho tunatakiwa kukifanya, lakini vyama vingine vilikuwa vinataja taja tu, lakini sisi tulisema wazi wazi kwamba ili kuondokana na rushwa na ufisadi ni lazima kurejesha miiko ya uongozi,” alisema.

No comments:

Post a Comment