KOCHA MPYA wa Timu ya Taifa ya Argentina Edgardo Bauza ameanza kwa kuweka mkakati wa kumrubuni Lionel Messi arejee tena kuichezea Nchi yake baada ya Mwezi uliopita kutangaza kustaafu.
Jana Bauza alithibitishwa na Chama cha Soka cha Argentina, AFA, kumbadili Gerardo Martino aliejiuzulu Mwezi uliopita baada ya kushindwa kwenye Fainali ya Copa America walipobwagwa na Chile kwa Mikwaju ya Penati huko USA ikiwa ni mara ya pili kwa Miaka Miwili mfululizo kutolewa na Chile kwa Penati katika Fainali ya Copa America.
Mara baada ya pigo hilo nae Messi akatangaza kustaafu kuichezea Argentina.
Bauza ameeleza amepanga kuongea na Messi kumwelezea mikakati yake kulifufua upya Soka la Argentina.
Bauza, ambae aliamua kuondoka Klabu ya Sao Paulo ili kuifundisha Argentina, atasaini Mkataba wa kuwa Kocha wa Timu ya Taifa ya Argentina hapo Ijumaa.
Mara baada ya hilo, Bauza atabakiza Wiki chache kuchagua Kikosi chake cha kwanza kabisa ambacho kinatakiwa kucheza Nyumbani na Uruguay na Ugenini na Venezuela mwanzoni mwa Septemba zote zikiwa Mechi za Kundi la Nchi za Marekani ya Kusini linalosaka Timu 4 zitakazotinga Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2018 huko Russia.
Baada ya Mechi 6, Argentina wapo Nafasi ya 3 katika Kundi hilo la Nchi 10 wakiwa Pointi 2 nyuma ya Uruguay na Ecuador.
Akiongelea kuhusu Kikosi cha Argentina, Bauza amesema hatabadili sana Kikosi hicho huku pia akifungua milango kwa Carlos Tevez, ambae alikuwa akitemwa na Makocha waliopita wa Argentina, kurejea tena Kikosini.
Bauza ameeleza: “Namfikiria Tevez kama Wachezaji wengine…Tevez ni Mchezaji mzuri kuichezea Timu ya Taifa.”
No comments:
Post a Comment