Makundi
ya kutetea haki za kibinadamu ya kitaifa na kimataifa yanataka uchunguzi
kufanywa kuhusu mauaji ya kiholela yanayodaiwa kufanywa na vyombo vya
usalama dhidi ya raia. Hii ni baada ya kuuawa kwa wakili.
Maafisa
nchini Kenya lazima wachunguze kwa dharura mauaji ya watu watatu wiki
jana, akiwemo wakili wa kutetea haki za kibinadamu, na wale
watakaopatikana na hatia wachukuliwe hatua mahakamani. Hayo yamesemwa na
mashirika 34 ya kitaifa na kimataifa yanayotetea haki za kibinadamu.
Wito huu
unajiri huku wanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu wakifanya
maandamano jijini Nairobi na miji mingine ya Kenya kuyalaani mauaji hayo
ya kikatili.
Wakili
Willie Kimani, mteja wake na dereva wake walitekwa nyara, wakatoweshwa
na baadaye kupatikana wameuawa na miili yao kutupwa katika mto, kilomita
73 kaskazini mashariki ya Nairobi. Watetezi wa haki za kibinadamu
wanasema hali hiyo inaibua hofu kuhusu hali ya haki za kibinadamu na
uzingatifu wa sheria nchini Kenya, hasa ikizingatiwa kuwa ripoti
zinaonyesha maafisa wa polisi walihusika.
Haya
mauaji ya kiholela ni ukumbusho wa kuwa haki ya kutafuta haki ya
kibinadaamu inakiukwa na inevunjwa. Amesema Muthoni Wanyeki ambaye ni
mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za kibinadamu Amnesty
International katika maeneo ya Afrika Mashariki, Pembe ya Afrika na
Maziwa makuu.
Ameongeza
kuwa afisi huru inayochunguza matendo ya polisi IPOA, lazima ianzishe
uchunguzi wa kipekee na huru kwa haraka kuhusu, utekaji nyara,
kutoweshwa na kuuawa kwa watatu hao, kwa dhamira ya kuwafungulia
washukiwa mashtaka.
Mwili wa
wakili Willie Kimani, ambaye alikuwa mwajiriwa wa shirika la kutetea
haki za kibinadaamu na misaada International Justice Mission lenye makao
yake makuu nchini Marekani, pamoja na miili ya dereva wake na wa mteja
wake Josephat Mwenda ilipatikana katika mto Ol-Donyo Sabuk katika kaunti
ya Machakos, mashariki ya Kenya tarehe 30 mwezi Juni. Hiyo ikiwa ni
wiki tatu baada ya watatu hao kutoweka kwa njia ya kutatanisha.
Polisi washukiwa kuhusika
Ripoti za
awali zilidokeza kuwa afisa mmoja wa polisi wa utawala, ambaye
alimshtaki Menda huenda ndiye aliwateka nyara. Watatu hao walionekana
mara ya mwisho wakitoka katika mahakama ya Mavoko kaunti ya Machakos
tarehe 23 Juni 2016 baada ya kusikizwa kwa kesi yao.
Maafisa
wa polisi wa utawala katika kituo cha Syokimau walimfungulia Mwendwa
kesi mnamo Disemba 2015, miezi kadhaa baada ya yeye kuwasilisha
malalamiko katika shirika huru la IPOA dhidi ya afisa mmoja mkuu wa
polisi ambaye alimpiga risasi bila hatia pale alipokuwa akishuka kwenye
pikipiki yake aliposimamishwa na maafisa wa polisi.
Makundi
ya kutetea haki za kibinadamu yamesema yanao ushahidi kuwa watatu hao
walizuiliwa katika kituo cha polisi wa utawala Syokimau muda mfupi kabla
ya ripoti za kutekwa nyara kwao kuibuka. Tangu hapo taarifa za wapi
walikuwa zilisalia kutojulikana hadi miili yao ilipopatikana siku saba
baadaye.
"Kwamba
mauaji haya yanajiri baada ya misururu ya madai sawa na hayo katika
maeneo mengine ya nchi kuchunguzwa, yanaibua swali tete la ikiwa maafisa
nchini Kenya wapo tayari kukomesha mauaji ya kiholela," amesema Henry
Maina ambaye ni mkurugenzi wa shirika la Article 19 katika Afrika
Mashariki. Amesisitiza kuwa rais Kenyatta laazima achukue hatua
madhubuti kuhakikishia wakenya na jamii ya kimataifa kuwa serikali
inachukuliwa kwa uzito suala la mauaji ya kiholela yanayofanywa na
polisi.
Polisi wazuiliwa rumande
Polisi
watatu wanaodaiwa kuhusika katika mauaji hayo walikamatwa na kufikishwa
mahakamani mapema leo. Hakimu mkuu Aniel Ogembo ameamuru washukiwa hao
Frederick Leliman, Stephen Chebulet na Sylvia Wanjiku kuzuiliwa kwenye
rumande kwa siku 14 ili kuruhusu uchunguzi kamili kukamilishwa.
Katika
muda huo, miili ya marehemu pia itafanyiwa uchunguzi kubaini aina ya
mapigo au dhuluma waliyotendewa kabla ya kufa au kutupwa mtoni.
Mkurugenzi wa tume ya kitaifa ya kutetea haki za kibinadamu Kenya George
Kegoro amesema mauaji hayo ya kikatili yanapaswa kuwa wito kwa rais
Kenyatta kubuni tume maalum kufanya uchunguzi dhidi ya polisi kama asasi
inayotumia visivyo nguvu na mamlaka yake, kwa manufaa ya kibinafsi au
kuendeleza uhalifu.
Mataifa
washirika wa Kenya hasa Sweden, Uingereza na Marekani yanayofadhili
polisi ya Kenya yametakiwa kushinikiza maafisa wa Kenya kuhakikisha
uchunguzi kamili umefanywa. Kufadhili vyombo vya usalama vya Kenya bila
kuhakikisha vinawajibika kulinda haki za kibinadamu hufanya mataifa
yanayofadhili pia kuchangia katika ukiukaji wa haki za kibinadamu.
Nao
mawakili nchini humo wametangaza mgomo wa wiki nzima. Wametsema
hawatafika katika mahakama kuwakilisha wateja wao, kama njia moja ya
kukemea mauaji ya mwenzao na mauaji ya kiholela kwa jumla yanayoendelea
nchini Kenya.DW
No comments:
Post a Comment