Thursday, 3 March 2016

SIMBA NA MBEYA CITY KIVUMBI JUMASOSI




Mbeya City vs Simba

Ligi kuu Tanzania bara inaelekea mzunguko wake wa 21 mwishoni mwa wiki hii kwa timu zote 16 kupambana katika kusaka alama tatu muhimu. Hadi sasa si rahisi kufahamu ni timu gani inaweza kutwaa ubingwa mwishoni mwa msimu lakini timu za Yanga SC, Azam FC na Simba SC mojawapo inaweza kushinda ubingwa huo.
Vita nyingine ni ile ya kuwania nafasi ya nne hadi ile ya 6 (nafasi ambayo huzifanya timu kuingia katika bodi ya ligi).
Vita kali nyingine msimu huu inataraji kuwepo katika eneo la kushuka daraja. JKT Ruvu, African Sports, na Coastal Union zinaweza kushuka endapo hazitafanya jihada kujinasua katika nafasi walizopo sasa (nafasi ya 16 kwa JKT Ruvu, nafasi ya 15 kwa Sports na nafasi ya 16 kwa Coastal kabla ya mechi za wikendi hii).
Hapa nakuletea uchambuzi na mtazamo wangu kuhusu VPL ilivyo na inavyoweza kuwa baada ya gemu za Jumamosi na Jumapili hii.
SIMBA SC v MBEYA CITY FC
Simba wapo mkoani Morogoro na wameweka kambi ya siku kadhaa kabla ya kurejea Dar es Salaam kuwavaa Mbeya City wikendi hii. Ushindi utawapeleka ‘Wekundu wa Msimbazi’ hadi kileleni mwa msimamo japo kwa masaa 24 tu.
City imekosa muendelezo wa matokeo mazuri msimu huu, walipoteza mchezo wa mzunguko wa kwanza katika uwanja wao wa nyumbani, Sokoine, Mbeya. Goli lisilotarajiwa na mlinzi wa kati, Mganda, Juuko Murshid mwanzo mwa mchezo huo lilisimama hadi mwisho na kuwapa Simba ushindi wa kwanza mbele ya City tangu timu hiyo ilipopanda VPL msimu wa 2013/14.
City haijawahi kupoteza mchezo dhidi ya Simba katika uwanja wa Taifa. Ilisawazisha mara mbili na kutengeneza sare ya 2-2 mwanzoni mwa msimu wa 2013/14, ikashinda 2-1 msimu uliopita walipoishinda Simba katika mechi zote mbili (2-1 uwanja wa Taifa na 2-0 uwanja wa Sokoine) lakini ili waendelee kupata matokeo mazuri katika mchezo ujao watapaswa kupandisha uwezo wao wa kujituma kwa mchezaji mmoja mmoja hadi timu kiujumla, kupunguza makosa mengi ya kizembe katika ngome yao dhaifu kwani wanakwenda kukutana na washambuliaji Hamis Kizza na Ibrahim Ajib ambao kwa pamoja wamekwishafunga jumla ya magoli 24.
Simba imetoka kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Yanga, lakini ushindi wa 5-1 dhidi ya Singida United mwishoni mwa wiki iliyopita ni kama umerudisha utulivu kikosini licha ya kwamba kumetokea kutoelewana kati ya nahodha msaidizi, Hassan Isihaka na kocha wake Mganda, Jackson Mayanja.
Kitendo cha kwenda Morogoro kuweka kambi ya muda kujiandaa na mchezo huo kitasaidia sana wachezaji kurudisha umakini baada ya kupoteza mchezo wa kwanza katika ligi baada ya kushinda gemu 6 mfululizo. Ikiwa nafasi ya 3 na pointi 45 baada ya kucheza michezo 20, Simba inapaswa kuwashinda City ili kushika usukani.
Wakati vinara Yanga SC (wenye michezo 19) watawavaa wanaoshika nafasi ya pili timu ya Azam FC (wenye michezo 19) siku ya Jumapili ni wazi Simba inapaswa kutumia mwanya huo kukaa juu ya timu mojawapo kufikia siku ya Jumatatu ijayo.
Kushindwa kuifunga City kwa mara nyingine katika uwanja wa Taifa kutadidimiza zaidi matumaini yao ya kushinda ubingwa. City inakuja kuwavaa Simba wakiwa nafasi ya kumi katika msimamo wakiwa na pointi 21.
Mayanja amesema City haiko katika nafasi mbaya lakini si kweli, kutokana na michezo iliyosalia na pointi ambazo timu 6 za juu walizokusanya na na uwiano mdogo kipointi uliopo kati ya timu ya 8 hadi ya 16 katika msiamamo ni wazi kikosi cha Mmalawi, Kinnah Phiri hakipo salama.
City imepitwa pointi 9 na Stand United iliyo nafasi ya saba, na imewapita kwa pointi 6 tu timu ya mwisho katika msiamamo, JKT Ruvu yenye pointi 15. Simba v City, mechi yenye malengo sawa, mtazamo mmoja, katika vita tofauti kwa maana kwamba, Ushindi ni muhimu katika kampeni za Simba kushinda ubingwa, na ni muhimu pia kwa City kwa maana kufungwa kutawafanya wawe hatarini zaidi.
Nani mshindi wa gemu hii? Haruna Moshi ‘Boban,’Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Abdallah Juma, watapaswa kupandisha viwango vyao vya kujituma ili kuendana na kasi ya kina Justice Majabvi, Jonas Mkude, Said Ndemla. Wachezaji hao wa zamani wa Simba wana vipaji vikubwa katika umiliki wa mpira, kupiga pasi za hatari na kufunga magoli ila wanacheza kivivu sana.
Wakichangamka na kupitisha pasi zao za hatari kwa kijana Raphael, Joseph Mahundi au Themi Felix bila shaka City wataendeleza rekodi yao ya kufunga walau magoli mawili dhidi ya Simba katika uwanja wa Taifa.
Haruna Shamte na Tumba Sued huwa wana mchezo wa kukamia, nachokipenda kwao hawapendi kupoteza mechi lakini wanapaswa kujiongoza wao wenyewe kwanza mchezoni na kupunguza rafu zao za wazi, vinginevyo wataadhibiwa na Kiza na patna wake Ajib na itakuwa mbaya zaidi kama wataiacha timu yao pungufu kwa kulambwa kadi nyekundu.
Wakati beki ya Simba iliyumbishwa sana na washambuliaji wa Yanga, Ciy wanaweza kuwachanganya zaidi, Emily Nimubona, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko na Majabvi kama tu viungo wao watacheza kwa nguvu na pasi za uhakika. Hii ni vita ya kwenda kileleni upande wa Simba, na itakuwa vita ya kukimbia eneo la hatari la kushuka daraja upande wa City. Tarajia mechi kali na ngumu zaidi kwa wenyeji Simba.

No comments:

Post a Comment