Tuesday, 16 February 2016

MAMA ALIYEMTIMUA MAXIMO JUMAMOSI KUZIHUKUMU SIMBA, YANGA

 
MWAMUZI Mwanamama, Jonesia Rukiyaa mwenye Beji ya FIFA anaetoka Kagera amekabidhiwa jukumu la kuwa Mwamuzi wa kati kwenye Mechi ya Ligi Kuu Vodacom, VPL, baina ya Yanga na Simba, mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam hapo Jumamosi.
Rukyaa ndiye aliyechezesha pambano la mwisho la Nani Mtani Jembe Simba SC ikiifunga Yanga SC 2-0 Mwaka juzi kwa Mabao ya Awadh Juma na Elias Maguri na Matokeo hayo yalisababisha Yanga imtimue Kocha wake Mbrazil Marcio Maximo.
Katika mchezo huo  Jonesia atasaidiana na Josephat Mburali (Tanga) na Samwel Lupenzi (Arusha) huku Mwamuzi wa Akiba akiwa  Elly Sasii wa Dar es Salaam, wakati Kamisaa atakuwa Mshambuliaji wa zamani wa Pamba ya Mwanza, Khalid Bitebo 'Zembwela'.
Rukyaa ambaye ana umri wa miaka 26, aliwahi kuweka rekodi ya kipekee FIFA Mwaka jana kwa kuwa Mwamuzi wa kati wa kike aliye na umri mdogo zaidi kwenye orodha ya Waamuzi wa kati wanaotokea Afrika.
Mwamuzi huyo ambaye pia aliweka historia kwa kuwa Mwamuzi wa kwanza wa Kike kuchezesha mchezo wa watani Simba na Yanga, pia ameweka rekodi nyingine Tanzania ya kuwa Mwamuzi wa kati wa kike mdogo zaidi kuwahi kupewa Beji hiyo ya FIFA kutoka hapa Nchini.
Tangu mwaka 2006, Tanzania imewahi kuwa na Waamuzi watatu wa Kike wa kati waliowahi kupata Beji hiyo ingawa kwa mujibu wa Chama cha Waamuzi Tanzania (FRAT), Waamuzi hao walikua na umri mkubwa kuliko wa Jonesia.
Waamuzi wa kati waliowahi kupewa beji hiyo ni Flora Kashaija wa Dar es Salaam, Isabela Kapera wa Dar es Salaam na Judith Gamba wa Arusha.
Wakati huo huo Msemaji wa Shirikisho la soka la Tanzania (TFF) Baraka Kizuguto, ametangaza viingilio vya mchezo huo huku kiingilio cha chini kikiwa ni shilingi 7,000  na kile cha juu kikiwa ni Shilingi 30,000 ambapo tiketi zitaanza kuuzwa kwenye maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema kuwa litaimarisha ulinzi kwenye mchezo huo kwa lengo la kuhakikisha wanaofika kuangalia mchezo huo wanakuwa salama.
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Siro,  alisema kuwa jesho hilo limejipanga kikamilifu ili kuhakikisha mambo yanakwenda sawa siku ya mchezo huo.
“Jeshi limejipanga kikamilifu kuhakikisha hakuna matendo ya kiuhalifu ambayo yataweza kuvunja amani mahali hapo iwe ndani au nje ya uwanja, tunaamni mpira ni burudani huvyo yoyote atakayeweza kuwa kinyume na mtazamo wa wengi atakuwa anasababisha vurugu hatutaweza kumvumilia,” alisema nyota Kamanda Sirro.

No comments:

Post a Comment