Mahakama ya Shirikisho la Brazil huko Mjini Sao Paulo imetangaza kutoa amri ya kuziweka chini ya ulinzi Mali za Nahodha wa Brazil na Mchezaji wa Barcelona ya Spain, Neymar.
Mali hizo za Supastaa huyo zina thamani ya Pauni Milioni 34.5 na ni pamoja na Merikebu ya kifahari, Ndege na Mali nyingine kadhaa.
Amri hiyo inatokana na Neymar, mwenye Miaka 23, kushitakiwa kwa Kosa la Ukwepaji Kodi katika kipindi cha kati ya 2011 na 2013.
Mwenyewe Neymar amekana kuhusika na kosa lolote.
Miongoni mwa Mali zilizoambatanishwa kukamatwa ni Makampuni Matatu yanayomilikiwa na Familia ya Neymar.
Waendesha Mashitaka wa Brazil wanadai Neymar alifungua Kampuni kadhaa ili zimkinge na alipe kiwango kidogo cha Kodi kupita anachostahiki na sasa wanadai Brazil ilipwe Pauni Milioni 11 ya Kodi ambayo alikwepa kulipa.
Mahakama imezipiga tanji mali hizo za Neymar ili kuhakikisha analipa kiasi anachodaiwa pamoja na Faini yeyote atakayotozwa.
Wataalam wa Kodi huko Brazil wamedokeza kuwa Neymar ana haki kukata Rufaa kupinga Amri hizi na pia adhabu hii haitakuwa na Kifungo cha Jela.
Wataalam hao wamesema kuwa ikiwa Neymar atalipa kiasi anachodaiwa basi Kesi itafungwa hapo hapo.
Mapema Mwezi huu, huko Spain, Neymar na Baba yake, walihojiwa Mjini Madrid Nchini Spain kuhusu madai ya rushwa na udanganyifu kuhusiana na Uhamisho wake kutoka Klabu ya Sao Paulo ya Brazil kwenda Barcelona ya Spain Mwaka 2013.
Kwenye hilo nalo, Neymar amekana kuhusika na kosa lolote.
No comments:
Post a Comment