Tuesday, 1 December 2015

TRA YAKAMATA MAKONTENA

Image result for MAKONTENA
   MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imekamata makontena tisa, yaliyotoroshwa kutoka katika bandari kavu na kuhamishiwa katika eneo la Mbezi Tangi Bovu, Dar es Salaam, hivyo kuwepo na kiashiria cha ukwepaji wa kodi.
Akizungumza katika eneo la tukio, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alisema kontena hizo zilikamatwa usiku wa kuamkia jana kwa ushirikiano na polisi.
Kayombo alisema makontena hayo, yanaonekana kuhamishwa kutoka katika bandari kavu ya PMM iliyopo Vingunguti katika Manispaa ya Ilala na kuhamishiwa katika eneo, ambalo linaonekana kuendelezwa kama bandari kavu, lakini halipo katika orodha ya TRA.
Aidha, alisema kibali cha makontena hayo kutoka bandarini kinaonesha kuwa yalitakiwa kutoka tangu Septemba 17, mwaka huu na kupelekwa eneo la Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) Ubungo, lakini cha kushangaza yametolewa usiku wa kuamkia jana na kupelekwa katika eneo ambalo si rasmi, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu kutokana na muda wake kupita.
“Kibali chake kinaonesha yalitakiwa yatoke tangu Septemba 17, mwaka huu, lakini yametoka usiku wa kuamkia leo (jana) na yalikuwa yanatakiwa kwenda EPZA pale Ubungo, lakini yamekuja huku, kwa maana hiyo hapa kuna kiashiria cha ukwepaji wa kodi,” alisema Kayombo.
Hata hivyo, haikujulikana mara moja vitu vilivyokuwemo ndani ya makontena hayo kutokana na kutofunguliwa kwanza hadi wahusika watakapopatikana ndipo yafunguliwe. “Mpaka sasa hatujajua ni kitu gani kilichomo kwenye haya makontena, tunachokisub
iri ni wakala au mmiliki wa mizigo hii ajitokeze ili yafunguliwe mbele yake,” alisema Kayombo.
Alisema kwa mujibu wa sheria na taratibu za forodha ni lazima makontena hayo, yafunguliwe mbele ya mmiliki au wakala wake wa forodha. Hata hivyo, watu hao wasipojitokeza ndani ya saa 24 kuanzia jana asubuhi wana uwezo wa kuchukua hatua.
Kayombo alibainisha hatua wanazoweza kuchukua ni pamoja na kufungua makontena hayo, kuyataifisha na kama bidhaa zilizoko ndani yake ni halali, zitanadiwa na kama ni haramu zitateketezwa.
Kayombo alisema kwa mujibu wa nyaraka za makontena hayo zinaonesha kuwa mizigo hiyo iliagizwa na Kampuni ya Heritage Empire Company Limited na wakala wa forodha ni Nipoc Africa Company Limited.
Alisema waliweka alama maalumu katika makontena hayo ili kuonesha kuwa yapo chini ya ulinzi na pia eneo hilo na malori manne yaliyotumika kubeba makontena hayo na madereva wake wako chini ya ulinzi kwa uchunguzi.
Kwa upande wake, Meneja wa TRA Bandarini, Ben Usaje alisema walipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuhusu uwepo wa makontena wanayohisi yameingia nchini bila kulipiwa ushuru.
Usaje alisema baada ya kupata taarifa hizo, walifuatilia kwa kushirikiana na polisi na kubaini kuwepo kwa makontena hayo katika eneo hilo, ambapo waliliweka chini ya ulinzi kwa hatua zaidi.
Alisema wanashangazwa na kitendo cha kukuta makontena hayo, yakiwa katika eneo linalofanana na bandari kavu, lakini sio rasmi na pia likiwa katikati ya makazi ya watu. “Mzigo ulitakiwa kuwa ICD, lakini inashangaza kuona umeletwa hapa katikati ya makazi ya watu,” alisema Usaje.
Makontena hayo yalibebwa katika malori yenye namba za usajili T891 CVX likiwa na tela lenye namna T831 CVZ, T877 CVY na tela lake namba T989 DDG, T838 CVX tela namba T553 DDC na T850 CVY na tela namba T546 DDC.
Aidha, madereva wa magari hayo walipoulizwa kuhusu kilichomo katika makontena hayo, walidai kuwa hawana nyaraka muhimu za kuonesha bidhaa zilizobebwa katika makontena hayo.

No comments:

Post a Comment