KASI ya utendaji na udhibiti wa matumizi ya Serikali, ikiwemo kusimamia ipasavyo Serikali hasa ukusanywaji wa mapato ya Rais John Magufuli na Serikali yake, umeigusa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kamati hiyo, imebainisha wazi kuunga mkono na kumpongeza Rais Magufuli kwa kasi nzuri, aliyoanza nayo katika utekelezaji wa Ilani ya CCM na ahadi za Rais huyo alizozitoa katika kipindi cha kampeni za uchaguzi.
Pia kamati hiyo imewataka viongozi na watendaji wa Serikali, kuiga jitihada na kasi hiyo ya Dk Magufuli katika kufanyakazi na kuwaletea maendeleo wananchi. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu namna kamati hiyo, ilivyopokea taarifa ya utendaji wa Serikali katika utekelezaji wa Ilani ya chama hicho ya mwaka 2015/ 2020, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema kamati hiyo, inaunga mkono hatua zote zilizochukuliwa na Rais huyo ikiwemo kudhibiti matumizi ya Serikali.
“CC inaunga mkono na kumpongeza Dk Magufuli kwa juhudi zake kubwa na kuhakikisha kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) zinasimamia ipasavyo ukusanyaji wa kodi za Serikali,” alisema Kinana.
Alisema kama ilivyoagizwa na Ilani yao, Serikali hiyo imeanza vizuri na kwa kasi katika kusimamia udhibiti wa matumizi yasiyo ya lazima ndani ya Serikali, ili kutumia fedha hizo kwenye utoaji wa huduma kwa wananchi.
Alisema kamati hiyo inaunga mkono juhudi hizo na kuwataka wote wanaohusika kwa namna moja au nyingine na udhibiti wa matumizi hayo, wamuunge mkono Dk Magufuli na Serikali yake, ili kufanikisha lengo hilo.
Aliwataka wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla, kumuunga mkono Rais Magufuli na Serikali yake kwa kuitikia wito wa kufanyakazi kwa bidii, kwa maarifa na uzalendo. “Kamati Kuu inawahimiza watu wote kwenye maeneo yao ya kazi kujituma na kuchapa kazi ili kujenga nchi yetu na kumuunga mkono Rais Magufuli,” alisisitiza.
Katika eneo la kuhimiza uwajibikaji katika Serikali, taasisi na mashirika yake, Kinana, alisema katika kipindi cha muda mfupi, Dk Magufuli amefanikiwa kuhakikisha kuwa kunakuwa na uwajibikaji mkubwa serikalini, jambo litakaloboresha huduma za umma kwa njia endelevu.
Alisema juhudi hizo za Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Dk Magufuli, zimeleta matumaini mapya kwa sehemu kubwa ya wananchi na kukuza imani kwa Serikali yao. Aliwataka viongozi wengine kuiga mfano huo na kuhakikisha wanatimiza wajibu wao ipasavyo ili kutekeleza kwa haraka Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuleta maendeleo nchini.
Akijibu swali kuhusu taarifa zilizozagaa kwamba kasi hiyo ya Dk Magufuli haiendani na Ilani ya CCM, bali inafuata sera za upinzani, alisema maneno hayo ya upinzani yametolewa kwa lengo la kujipoza maumivu kutokana na ukweli kwamba tayari wameshindwa na hawana la kusema.
“Haya yote anayotekeleza Rais Magufuli yamo ndani ya Ilani ya CCM. Unajua kwenye uchaguzi kulikuwa na ushindani sasa sisi tumeshinda wenzetu wameshindwa, nawashangaa wanavyodai eti Rais anatekeleza sera zao, ninavyoona mimi huku ni kujipoza maumivu tu,” alisisitiza Kinana.
No comments:
Post a Comment