KOMBE LA DUNIA kwa Klabu linaanza huko Japan Alhamisi Desemba 10.
Washiriki wa Mashindano haya ni Barcelona, Mabingwa wa Ulaya, River
Plate, Mabingwa wa Marekani ya Kusini, America ambao ni Mabingwa wa
Nchi za Marekani ya Kati na Kaskazini na Visiwa vya Carribean, Mabingwa
wa Afrika TP Mazembe, Guangzhou Evergrande, Mabingwa wa Asia na Bingwa
wa Kanda ya Oceania.
Pia wapo Sanfrecce Hiroshima, Klabu Bingwa ya Japan, inayoshiriki kama Wenyeji wa Mashindano.
Wakati Barcelona wakiwa ndio wanategemewa kutwaa Kombe hili
wakijivunia Kikosi chenye Masupasta Lionel Messi wa Argentina, Nahodha
wa Brazil Neymar na Straika wa Uruguay Luis Suarez, Tanzania itaikodolea
macho TP Mazembe yenye Mastraika Wawili mahiri kutoka Nchi hiyo, Mbwana
Samatta na Thomas Ulimwengu.
Mwaka 2010, TP Mazembe ilifika Fainali ya michuano hii na kufungwa na Inter Milan.
Klabu ya China, Guangzhou Evergrande, pia itakodolewa macho kwa
vile Kocha wao ni Mbrazil Luiz Felipe Scolari ambae aliisaidia kutwaa
Ubingwa wa Asia.
Mechi ya ufunguzi ya Alhamisi ni kati ya Wenyeji Sanfrecce
Hiroshima ikicheza na Auckland City katika Raundi ya Awali ambapo
Mshindi atatinga Robo Fainali kucheza na TP Mazembe, inayoanzia hatua
hii na Mechi hii itachezwa Jumapili huko Osaka.
Mshindi wa Robo Fainali hii atatinga Nusu Fainali kucheza na River Plate itakayoanzia hapo.
Katika Robo Fainali nyingine hapo Jumapili America itaivaa
Guangzhou Evergrande na Mshindi wake kwenda Nusu Fainali kuikabili
Barcelona itakayoanzia hapo.
No comments:
Post a Comment