Mwangalizi wa uchaguzi wa kimataifa, kutoka ubalozi wa Ubelgiji
nchini, Paul Cartie, alisema upigaji kura ulienda vizuri japo katika
baadhi ya maeneo ulifanyika kwa taratibu sana.
Alisema katika baadhi ya vituo alivyotembelea alishuhudia mtu mmoja
akitumia hadi dakika 10 kupiga kura na kuwafanya watu wengine kusubiri
zamu zao kwa muda mrefu.
Alisema amefurahishwa na mwamko mkubwa ulioonyeshwa wa Watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura.
Akizungumza na waandishi wa habari alipotembelea kituo cha kupigia
kura cha Shule ya Msingi Osterbay, jijini Dar es Salaam, Muangalizi Mkuu
wa Uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya (EU), Judith Sargentini, alisema
wametembelea vituo 400 mijini na vijijini na kwamba katika maeneo hayo
yote wameshuhudia uchaguzi umeenda vizuri licha ya kuwapo kwa changamoto
ndogondogo.
Hata hivyo, alisema ripoti kamili kuhusiana na uchaguzi wanatarajia kuitoa leo.
Kwa upande wake, Mwangalizi Mkuu wa Uchaguzi kutoka Jumuiya ya
Madola, Rais wa zamani wa Nigeria, Goodluck Jonathan, alisema
hazungumzii lolote mpaka leo watakapotoa ripoti yao.
JIMBO LA KAWE
Mgombea ubunge Jimbo la Kawe kupitia Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Halima Mdee, alisema katika kituo cha Makongo Juu
alikopigia kura, kulikuwa na dosari mbalimbali zilizojitokeza katika
maeneo mengi ikiwa ni pamoja na ucheleweshwaji wa vifaa.
Naye mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Kippi Warioba, ambaye alipiga kura katika kituo cha Ununio,
alilalamikia makarani wanaoandikisha wapiga kura kuendesha kazi hiyo
taratibu.
No comments:
Post a Comment