![]() |
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela |
Watu wanne wanashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wakidaiwa kutaka kuteka magari yaliyobeba vifaa vya kupigia kura.
Miongoni mwa vifaa hivyo ni masanduku yaliyokuwa na karatasi za
kupigia kura na kwamba tukio hilo lilitokea eneo la Darpori wilayani
Nyasa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela, alisema jana
kuwa maafisa wa serikali waliokuwa wakisafirisha vifaa hivyo walibaini
kuwekewa vizingiti barabarani na waliposimama, watu hao walitoka porini
na kuwazingira.
Kamanda Msikhela alisema ‘wavamizi’ hao walikuwa wameshika mapanga
na silaha za jadi lakini walidhibitiwa na askari polisi waliokuwa kwenye
msafara huo.
Katika tukio jingine, askari polisi katika manispaa ya Songea
wametumia mabomu kuwatawanyisha watu walioandamana na kuifunga barabara
ya kutokea mjini humo kwenda Mbinga.
Mtu mmoja ambaye jina lake halikupatikana mara moja anashikiliwa na
polisi akihusishwa na kuwashambulia askari polisi waliokuwa wakidhibiti
maandamano hayo. Kwa mujibu wa Msikhela, polisi inawatafuta watu
wengine wanaodaiwa kuandamana isivyo halali na kusababisha vurugu kwa
kuifunga barabara hiyo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela, aliwaambia
waandishi wa habari mjini hapa jana kuwa, tukio la kuandamana lilitokea
juzi katika eneo la Lizaboni mjini humo. Msikhela alisema maandamano
hayo yalifanyika baada ya kumalizika kwa mkutano wa mwisho wa kampeni za
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Alisema maandamo hayo yaliyomshirikisha pia mgombea ubunge wa
Songea Mjini kupitia Chadema, Joseph Fuime, yalianzia eneo walilofanya
mkutano na kwamba polisi ilipowataka watawanyike walikaidi.
“Baada ya wafuasi hao kutotii amri halali ya Jeshi la Polisi, tuliamua kutumia nguvu kutawanya maandamano hayo,” alisema.
Licha ya kuandamana, Msikhela alisema washiriki wa maandamano hayo
waliwajeruhi askari polisi wanne kwenye sehemu mbalimbali za miili yao.
Alisema askari hao ambao hakuwataja majina walishambuliwa kwa mawe.
Msekhela alisema polisi inaendelea kupeleleza zaidi kuhusu tukio hilo
la Fuime.
No comments:
Post a Comment