Thursday, 22 October 2015

KASORO 300 ZABAINISHSWA KATIKA DAFTARI KA KUDUMU LA WA PIGA KURA


 



Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imesema uchakataji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura umekamilika na wamebaini kasoro ndogo ndogo takriban 300 ambazo zimeondolewa.

Mkurugenzi wa Daftari na Tehama wa Nec, Dk. Modest Kipilimba, alisema walianza na kasoro 17 zilizobainishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Ukawa walibainisha kasoro hizo katika kituo cha mpigakura cha Ofisi ya Kitongoji Azimio 1, chenye namba 10101010102, kilichopo mtaa wa Mahoma/Makulu, Kata ya Chahwa, jimbo la Dodoma Mjini.

Ukawa walibainisha vivuli, mabati, hoteli, watu waliojipiga picha wenyewe, Wazungu, Wachina na vivuli vikiwa vimepewa namba ya mpigakura na majina yasiyoeleweka.
“Tumeondoa kasoro nyingi sana na kituo cha Azimio kwa sasa hakuna kasoro yoyote, mbali na kasoro hizo, kasoro nyingi ni za jinsia, kujirudia, jina kutokuonekana, majina kukosewa kulingana na wananchi wanavyopiga simu katika kituo chetu kilichopo Nec,” alisema.
Aidha, alisema ni vugumu kueleza kasoro hizo zilibainika katika vituo vingapi, lakini kwa sasa vyama husika vimekabidhiwa Daftari ambalo halina kasoro zozote.
“Daftari limeshapelekwa katika vituo mbalimbali na limebandikwa, wananchi wanapokwenda kwenye vituo kuangalia taarifa zao wanapoona hazipo wanaruhusiwa kuwasiliana nasi moja kwa moja kupitia ‘Calling center’ yetu, apige namba 0800782100 ili kupata msaada, nasi tunarekebisha taarifa zake,” alifafanua Dk. Kipilimba.
Alisema marekebisho yataendelea kwa kadiri wananchi wanavyopiga simu kwa kuwa ni jambo la kawaida kuchanganya majina ambayo siyo rahisi kuyabaini kama ni ya kike au kiume kwa kuwapa jinsia halisi.
Dk. Kipilimba alisema kasoro nyingine ni za waliojiandikisha zaidi ya mara moja kwa kuwa wapo ambao wamejiandikisha mara nane, lakini Daftari la mwisho linapaswa kumtambua mtu mmoja.
Mkurugenzi huyo alisema vyama vyote vimeshapewa Daftari lingine ambalo limekamilika na vinaruhusiwa kuwasilisha kasoro watakazoziona kwa kuwa kasoro nyingi ni za kawaida na za kibinadamu zaidi.
Alisema kuwa kasoro hizo hazitabadili idadi ya wapigakura kwa kiasi kikubwa na kwamba haitazidi 100 kwani hadi sasa wenye sifa ya kupiga kura ni 22, 751,292.
Awali baada ya kukamilika uandikishaji wapigakura Nec ilisema watu wenye sifa ya kupiga kura ni zaidi ya milioni 23.78, na baada ya uchakataji ilibainika watu milioni 22.75 ndiyo wapiga kura halali.

No comments:

Post a Comment