Sunday, 5 June 2016

Hotuba ya Zitto Kabwe katika uzinduzi wa “Operesheni Linda Demokrasia Nchini”.

Ndugu Wananchi, Nawashukuru sana kwa kujitokeza kwenu kuitikia wito wetu wa kuja kutusikiliza. Tumewaita hapa ili kuwaeleza kinachoendelea katika nchi yetu hivi sasa na madhara makubwa yanayoweza kutokea iwapo hatutosimama kidete dhidi ya mbinu zozote za kufifiza na kuminya demokrasia na misingi ya uwajibikaji katika nchi yetu.

Mwaka 2015 tulikwenda kwenye uchaguzi kuchagua madiwani, wabunge na Rais. Baada ya Uchaguzi kumalizika Serikali mpya iliundwa na Serikali za Mitaa (Halmashauri) kuundwa. Nawapongeza wananchi wote kwa kuendesha zoezi la uchaguzi kwa amani na kuweka heshima ya nchi yetu mbele.

Baada ya uchaguzi tumeona viongozi wapya wakichukua hatua mbalimbali nzuri na mbaya, zenye kujenga na kubomoa, zenye kuimarisha demokrasia na zinazobomoa demokrasia. Tumeshuhudia maamuzi mengine ambayo yanatia khofu, kwamba ingawa tunaona dhamira ya dhati ya kupambana na Ufisadi, lakini pia tunaona mbinu za chini chini za kutokomeza Demokrasia ya nchi yetu ambayo tumeijenga kwa jasho na damu.

Mkutano wetu wa leo utagusia baadhi ya maeneo ambayo tunadhani ni vihatarishi vya ustawi wa wananchi wetu na ambavyo lazima tuanze kuvipinga mapema sana kabla havijaota mizizi. Ndugu Wananchi, Baadhi ya maeneo tutakayozungumza leo ni pamoja na;
  1. Wabunge kusimamishwa kazi za Bunge
  2. Maamuzi ya Serikali kuhusu Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma
  3. Hali ya Zanzibar
  4. Mwelekeo wa Bajeti ya Kwanza ya Serikali ya Rais Magufuli
  5. Tishio la Nchi kuelekea kwenye Utawala wa Imla wa MTU mmoja
Wabunge Kusimamishwa Kazi.
Ndugu Wananchi, mnamo tarehe 30 Mei, 2016 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Naibu Spika lilipitisha Azimio la Bunge la kuwasimamisha kazi wabunge 7 kwa vipindi mbalimbali. Wabunge wawili, ndugu Esther Bulaya na ndugu Tundu Lissu walisimamishwa Mikutano miwili ya Bunge. Wabunge Wanne, ndugu Halima Mdee, Ndugu Pauline Gekul, Ndugu Godbless Lema na Mimi ninayezungumza nanyi tulisimamishwa mkutano mmoja, huu unaoendelea wa Bajeti, na mbunge mmoja ndg John Heche Suguta amesimamishwa vikao 10 vya mkutano huu wa tatu unaoendelea.

Sababu iliyoelezwa na Bunge ni kwamba wabunge hawa walifanya fujo siku ya tarehe 27 Januari, 2016 kufuatia hoja niliyoitoa Bungeni ya kutaka mjadala kuhusu sababu za hovyo na za uongo zilizotolewa na Serikali kuhusu uamuzi wa kuzuia Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) pamoja na televisheni binafsi (Star tv na Azam) kuonyesha moja kwa moja mikutano ya Bunge.

Ndugu Wananchi, mimi binafsi pamoja na wabunge wengine 6 hatukufanya fujo yeyote ndani ya Bunge. Kosa letu kubwa ni kutaka kuhoji maamuzi ya Serikali ambayo kwa maoni yetu hayana msingi wowote. Serikali inasema ninyi Wananchi hamfanyi kazi kwa sababu Bunge linaonyeshwa wakati wa kazi. Hata hivyo Serikali hiyo hiyo inatwambia kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita uchumi wa Tanzania ulikua kutoka tshs 16 trilioni mwaka 2005 mpaka tshs 99 trilioni mwaka 2015. Kipindi chote hiki Bunge lilikuwa linaonyeshwa moja kwa moja na televisheni ya Taifa (TBC) na televisheni ya StarTV.

Kama mngekuwa hamfanyi kazi Uchumi usingekua kwa kiwango hicho cha asilimia 600 ndani ya Muongo mmoja wa uongozi wa Rais Jakaya Kikwete. Utawala wa Rais John Magufuli unataka kutuaminisha kuwa ukiwa na Bunge ‘live’ watu hawafanyi kazi lakini uongozi uliopita umedhihirisha kwa ushahidi kuwa ukipanua demokrasia na kuwaonyesha wananchi kila kinachoendelea Bungeni uwezo wa kazi unaongezeka na uwezo wa wananchi kuwajibisha viongozi wao unaongezeka.

Hivyo Serikali kuamua kuficha Bunge ni mbinu za kuendesha Serikali kwenye giza ili kufanya maamuzi ambayo baadaye ionekane Serikali tu au Rais tu ndiye mfanya kazi. Ndio maana mikutano yote ya Rais anapohutubia huonyeshwa moja kwa moja lakini sio Bunge.

Wananchi, Wabunge wamesimamishwa kwa sababu ya kukataa Bunge kuendeshwa kwenye giza. Wabunge waliosimamishwa walisimama kidete kuhoji sababu za Serikali kufikia maamuzi hayo. Walitaka kujua kwanini Serikali imekuwa kigeugeu kwa kubadilisha badilisha sababu zake za kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge.

Wakati mmoja Serikali ilisema sababu ni gharama, kama ni hivyo ni kwanini walizuia StarTV na AzamTV kuonyesha moja kwa moja? Ni dhahiri wananchi Serikali inataka kuendesha mambo yake kwa uficho kwa sababu kuna maamuzi inataka kufanya na haitaki wananchi mjue mapema maamuzi hayo. Serikali inaturudisha nyuma badala ya kwenda mbele.

Wananchi, wabunge waliosimamishwa ni wabunge wenye uwezo wa kujenga hoja. Kuna wengine wamebaki Bungeni wenye uwezo mkubwa tu wa kujenga hoja, lakini hawa saba waliosimamishwa ni wabunge waliojidhihirisha kwa muda mfupi kwa baadhi yao kama ndugu Heche, kwamba wanaweza kusimamia hoja zao bila woga. Swali la kujiuliza ni, tukio ambalo limetokea mwezi Januari ni kwanini lifanyiwe mwezi Juni tena wiki moja tu kabla ya Waziri wa Fedha kuwasilisha Bungeni Bajeti ya Serikali?

Katika waliosimamishwa ni pamoja na Waziri Kivuli wa Fedha, ndg. Halima Mdee na Waziri Kivuli wa zamani wa Fedha ambaye anazungumza nanyi leo (Zitto Kabwe). Kuna nini? Nitawaeleza katika hoja ya Bajeti. Kimsingi Utawala wa Rais Magufuli umepanga kupandisha kodi za wananchi masikini na uliona uwepo wetu bungeni utatibua mipango yao.

Rais na wenzake ndani ya CCM hawapendi kusikia hoja zinazowapinga, hawana uvumilivu wa kukosolewa na hivyo walipanga kuhakikisha kuwa baadhi yetu hatutakuwepo kwenye mjadala wa Bajeti ili kufanikisha malengo yao ya kufanya maamuzi yatakayowandamiza wananchi. 
Nitaeleza vizuri hili baada ya muda kidogo. Hivyo nataka Watanzania wajue kuwa kusimamishwa kwetu ni ajenda maalumu ya Serikali ya Rais Magufuli kufunika mjadala wa Bajeti kwa sababu inajua kuwa tunajua inachopanga kufanya dhidi ya mafukara wa nchi yetu.

Sisi hatutakaa kimya, tutatumia wenzetu waliopo Bungeni kuyasema haya na pia tutazungumza na wananchi kuwaeleza pia. 
Tutatumia mikutano yetu mbalimbali bila kujali itikadi za vyama vyetu kuhakikisha kuwa Wananchi wanajua kila kinachoendelea na kuwataka kuunganisha nguvu kukataa udikteta unaonyemelea nchi yetu.

Wanafunzi 7800 Kufukuzwa Chuo Kikuu Cha Dodoma.
Ndugu Wananchi, mmesikia sakata la Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma waliokuwa wanasomea programu maalumu ya Ualimu wa Sayansi. Hawa ni watoto wa Watanzania masikini waliokubali kuacha kwenda Kidato cha Tano na cha Sita (A level) na kukubali kusomea diploma ya Ualimu ili wakawafundishe watoto wa masikini wenzao. Wanafunzi hawa hawakuanzisha wao program hii, ilianzishwa na Serikali na kupitishwa na Baraza la Mawaziri ambalo Rais Magufuli alikuwa mjumbe na alishiriki kikao hicho kwa mujibu wa kumbukumbu za Baraza la Mawaziri.

Rais Magufuli hakupinga mpango huu na aliubariki kama Wenzake walivyofanya na kuanza kutekelezwa. Lengo na program hii ni kuondoa tatizo la walimu wa masomo ya Sayansi. Tanzania ina uhaba wa walimu wa Sayansi 26,000 (Kwa Utafiti wa Mwaka 2014) na tukienda kwa utaratibu wa kawaida tutahitaji miaka 20 kuziba pengo hilo.

Program hii ilianzishwa ili kuziba pengo hili kwa muda mfupi, na vijana waliitikia wito huu wa kizalendo kuhakikisha wadogo zao hawakosi walimu siku za usoni. Serikali ya awamu ya Tano imewafukuza vijana hawa 7800 kutoka chuoni ndani ya masaa 24 kwa makosa ambayo sio yao.

Wananchi, hatusemi kuwa program haikuwa na kosoro. Zilikuwepo ikiwemo kudahili wanafunzi wengi zaidi ya ilivyotarajiwa na kudahili wanafunzi 88 kati ya 7800 ambao walikuwa na daraja la nne (Div 4) katika masomo yao. Lakini aliyedahili sio watoto hawa bali ni Serikali yenyewe, kwanini waadhibiwe watoto?

Bunge lilipotaka kujadili hoja hii au hata kuipeleka kwenye kamati ya Bunge kuifanyia uchunguzi na kutoa mapendekezo Naibu Spika alizuia hoja ya mbunge Joshua Nasari bila sababu za msingi. Wabunge wote bila kujali vyama vyao walitaka hoja ijadiliwe na kuweza kupata majawabu. Mbona wakati wa Uongozi wa awamu ya 4 tulijadili hoja ya mgomo wa madaktari na kisha kupelekwa kwenye kamati ya husika ya bunge kupata suluhisho la kudumu? Kwanini Utawala wa Rais Magufuli hautaki Bunge lifanye kazi yake? Mbona yeye Rais kaenda kujadili jambo hilo huko Chuo Kikuu mlimani?

Wananchi, Rais Magufuli anafikia kuita watoto wetu Vilaza? Rais huyu anayesema yeye ni Rais wa masikini anaita watoto wa masikini Vilaza. Vijana hawa Wazalendo waliojitoa muhanga kuacha kwenda kidato cha Tano ili wasome kuwa Walimu na kulea kizazi kijacho Rais wao anawaita vilaza. Rais sifa zimempanda kichwani. Rais Magufuli hana budi kuwaomba radhi vijana hawa na wazazi wao.

Kitaaluma Rais ni Mwalimu, anajua madhara ya kisaikolojia kufuatia maneno aliyoyasema. Ni sawa na Jenerali wa Jeshi anayetukana askari wake walio Mstari wa mbele. Hata Baba wa Taifa hakuthubutu kamwe kuita wanafunzi Vilaza hata kama walimuudhi kiasi gani.

Rais Magufuli anaongea mno, sio sawa kwa Kiongozi. Rais ajue kuweka akiba ya maneno. Yeye ni Kiongozi wa wote, wenye akili na Vilaza. Yeye anapaswa kuwa wa mwisho kuongea ili watu waweze Kukata rufaa kwake. Yeye akishaongea wananchi ‘aggrieved’ (walioonewa Au kukosewa) waende kwa nani? Waende kwa mungu?

Tunamtaka Rais awarudishe wanafunzi Hawa Chuoni mara moja na wale wanafunzi ambao itaonekana hawakuingia kwenye programu kihalali (ambao Ni 88 Tu) waondolewe badala ya kuadhibu watoto wote kwa makosa ya wachache ambao ni asilimia 5 tu ya wote. 
Makosa madogo ni mambo ya kawaida katika Jamii. Yeye Rais ni mfano mzuri wa hili kwani naye mbona aliteua Waziri mlevi na kurekebisha kwa kumfukuza peke yake?, mbona hakufukuza Baraza zima la mawaziri kwa ulevi wa Waziri mmoja?

No comments:

Post a Comment